UVCCM(W)SHINYANGA MJINI WATOA MKONO WA POLE KWA FAMILIA YA BODABODA ALIYEFARIKI KWA AJALI

UVCCM (W)Shinyanga Mjini Watoa Mkono wa Pole kwa Familia ya Bodaboda Aliyefariki kwa Ajali

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini imetoa mkono wa pole kwa familia ya kijana Daniel Seni, dereva bodaboda, aliyefariki dunia kufuatia ajali ya barabarani.
Ajali hiyo imetokea juzi majira ya saa 3 asubuhi katika barabara ya Bugoyi,ambapo marehemu aligongana uso kwa uso na gari baada ya kugonga baiskeli iliyokuwa imebeba mkaa, na kusababisha kifo chake papo hapo.

Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abdulaziz Sakala, amefika nyumbani kwa marehemu katika eneo la Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, kutoa mkono wa pole na kuwafariji wafiwa,akiwa ameambatana na Katibu wa Jumuiya hiyo.
“Tumesikitishwa na msiba huu mkubwa wa kijana wetu. UVCCM inatambua mchango mkubwa wa maafisa usafirishaji, hususan bodaboda, katika maendeleo ya jamii. Chama Cha Mapinduzi kipo pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu,” amesema Sakala.

Kwa upande wake, Katibu wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Naibu Katalambula, alitoa wito kwa madereva wa vyombo vya moto kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuepuka mwendokasi ili kuepusha ajali.

Mwili wa marehemu Daniel Seni umesafirishwa kwenda kuzikwa nyumbani kwao katika Wilaya ya Maswa, Mkoa wa Simiyu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464