ZIARA YA MAMA FULL BOX OPERESHENI YATUA STENDI YA MABASI MKOA WA SHINYANGA KUSIKILIZA KERO NA KUZITAFUTIA UFUMBUZI

ZIARA YA MAMA FULL BOX OPERESHENI YATOA STENDI YA MABASI MKOA WA SHINYANGA KUSIKILIZA KERO NA KUZITAFUTIA UFUMBUZI

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

JUMUIYA ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini imetembelea Stendi ya Mabasi ya Mkoa wa Shinyanga,kusikiliza kero na kuzitafutia ufumbuzi.

Miongoni mwa kero walizokumbana nazo ni kukithiri kwa mashimo pamoja na vyumba kuvuja.
Ziara hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya, Abdulaziz Sakala, ilifanyika leo Aprili 17, 2025, ikiwa ni sehemu ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia suluhisho.

Akizungumza kabla ya kuanza kusikiliza kero za wananchi, Katibu wa UVCCM Wilaya, Naibu Katalambula, amewataka wananchi kutoa maoni yao ili yafanyiwe kazi na kufikishwa kwa mamlaka husika.
Wananchi wameeleaza malalamiko mbalimbali,ambapo walilalamikia ubovu wa miundombinu ya stendi hiyo ikiwemo mashimo mengi yanayohatarisha vyombo vya usafiri, pamoja na vyumba vya biashara na ofisi ambazo zimechakaa na kuvuja wakati wa mvua.

“Tumechoka na hali ya stendi hii. Kuna mashimo kila kona, magari yanaharibika. Tunaiomba Serikali iingilie kati,” amesema Said Mgongo, mmoja wa mawakala wa mabasi.
Naye Daudi Lefi,amelalamikia vyumba vya biashara na Ofisi katika stendi hiyo kuwa ni vibovu, na mvua zinaponyesha huvujiwa.

“Kila siku tunalalamika, lakini hakuna kinachofanyika. Tunalipa kodi kila mwezi, lakini huduma ni duni,” amesema Daudi.
Akijibu kupitia simu, Meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko amekiri kuwepo kwa changamoto hizo na kueleza kuwa ufinyu wa bajeti umechelewesha ukarabati wa stendi hiyo.

Katibu wa UVCCM Katalambula,ametoa maelekezo kwamba kwa upande wa ubovu wa vyumba vya biashara, Afisa Biashara afike kwenye Stendi hiyo, azungumze na wafanyabiashara na hata kuingia nao makubaliano,wakarabati wenyenye vyumba hivyo na kukatana kwenye kodi kuliko kuendelea kuteseka hadi bajeti ipatikane.
Amesema kwenye changamoto ya mashimo,wamesema napo ufanyike ukarabati wa haraka.

Amesema kwamba kutoka na Stendi hiyo kuwa na Changamoto nyingi,watafanya mkutano Maalumu na kuwashirikisha viongozi wote wa manispaa ya Shinyanga,Stendi hiyo pamoja na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, kujadili kwa pamoja namna ya kuzitatua.

Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Shinyanga Mjini Abdulaziz Sakala, amesema kero zote ambazo zimewasilishwa juu ya stendi hiyo wamezichukua na watazifanyia kazi.
Amewataka pia vijana ambao wanafanya biashara kwenye Stendi hiyo,kwamba wachangamkie pia fursa za mikopo ya halmashauri asilimia 10 ambazo asilimia Nne hutolewa kwa vijana na wanawake na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu.

Amewataka pia wajiandae kushiriki kwenye uchaguzi mkuu 2025,pamoja na kumpigia kura nyingi za ushindi Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, ili apate ushindi wa kishindo na kuendelea kuwaletea maendeleo na utekelezwaji wa miradi ikiwamo ya kimkakati.

TAZAMA PICHA👇👇
Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Shinyanga Mjini Abdulaziz Sakala akizungumza.
Katibu wa UVCCM wilaya ya Shinyanga Mjini Naibu Katalambula akizungumza.
Diwani wa Ibinzamata Ezekiel Sabo akizungumza.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464