MKUU WA WILAYA YA KISHAPU ATOA SALAMU ZA PASAKA NA KUTOA ZAWADI KWA MAKUNDI MAALUMU

MKUU WA WILAYA YA KISHAPU ATOA SALAMU ZA PASAKA NA KUTOA ZAWADI KWA MAKUNDI MAALUMU

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi,ameungana na wananchi wa wilaya hiyo katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka kwa furaha na mshikamano,huku akitoa salamu za upendo na kuwatakia Pasaka njema.

Akizungumza wakati wa tukio hilo,Mhe. Masindi amesema kuwa Sikukuu ya Pasaka ni wakati muhimu wa kuungana na familia kwa furaha, upendo na mshikamano. Alisisitiza kuwa ujumbe mkuu wa Pasaka ni kusherehekea ufufuko wa Yesu Kristo kwa moyo wa matumaini na ukarimu kwa wote.
 "Heri ya Sikukuu ya Pasaka. Ni furaha iliyoje kukutana nanyi leo. Tunafahamu kuwa lengo letu ni moja tu—kufurahi pamoja, kula pamoja na familia zetu na kuhakikisha tunadumisha furaha katika familia zetu. Tunaamini Kristo amefufuka pamoja nasi," amesema Masindi.

Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu imegawa msaada wa zawadi kwa makundi maalumu ili kuyashirikisha katika furaha ya Pasaka. 
Zawadi zilizotolewa ni pamoja na mchele zaidi ya kilo 250, mbuzi mmoja na lita 40 za mafuta ya kupikia.

Mhe. Masindi alieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuonyesha mshikamano wa kijamii na kuwapa faraja wale wenye uhitaji katika kipindi hiki cha sikukuu ya Pasaka.

Katika salamu maalumu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, wananchi wa Kishapu walitakiwa Pasaka njema huku wakihimizwa kuongeza upendo na mshikamano ndani ya familia na jamii kwa ujumla.
“Mhe. Rais Samia anawapenda sana na anawasihi katika Pasaka hii tuzidishe upendo—upendo usio na mipaka,” alieleza Mhe. Masindi.

Kwa niaba ya makundi maalumu, James Japhet ametoa shukrani kwa Mkuu wa Wilaya pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan kwa zawadi walizotoa, akisema kuwa hatua hiyo imewapa faraja kubwa na kuwafanya wajisikie kuthaminiwa na kuunganishwa katika jamii.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464