KATAMBI ATOA MAMILIONI YA FEDHA KUUNGA MKONO MICHEZO YA JADI SHINYANGA
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MBUNGE wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,ametoa Shilingi milioni 3 kuunga mkono michezo ya Jadi,inayotarajiwa kufanyika katika Manispaa ya Shinyanga.
Michezo hiyo inatarajiwa kufanyika kuanzia Aprili 29 hadi Mei 2, 2025,ikihusisha Kata 12 za Manispaa ya Shinyanga,ambapo Katambi ndiyo mfadhili mkuu wa michezo hiyo itakayo gharimu sh.milioni 6.3 ambapo leo amekabidhi milioni 3.
Fedha hizo zimekabidhiwa leo Aprili 25 na Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini,Hamisa Chacha,kwa niaba ya Mbunge Katambi,katika ofisi za chama hicho.
Akizungumza wakati wa makabidhiano,Hamisa amesema michezo ya jadi ni muhimu katika kudumisha mila, tamaduni na maadili ya Mtanzania, hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya maeneo yameanza kusahau kabisa mizizi yao ya kiafrika.
“Michezo hii ya jadi ni muhimu sana hasa katika kulinda maadili ya Mwafrika, sababu kuna maeneo mengine yameanza kusahau kabisa Maadili ya kiafrika,”amesema Chacha.
Aidha,amesema kuwa michezo hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kumpongeza Mbunge Katambi kwa kuendelea kutekeleza ilani hiyo kwa vitendo.
Amewapongeza pia waandaaji wa michezo hiyo ya Jadi, kwamba watawakutanisha watu pamoja na kuenzi Mila na Tamaduni zao.
Kaimu Katibu wa Michezo ya Jadi Manispaa ya Shinyanga Leonard Mapolu, amesema michezo hiyo inalenga kudumisha utaifa, asili ya Mtanzania,maadili,na hata amani ya nchi.
Alitaja michezo itakayochezwa kuwa ni pamoja na Ngoma za Asili (Mbina),Bao,kupikicha Moto,kucheza na Nyoka,Fisi pamoja na kupiga Zeze.
Mwenyekiti wa Michezo ya Jadi wa Manispaa hiyo, Janeth Seseja, ametoa shukrani kwa Mbunge Katambi kwa kujitolea na kukubali ombi lao, akisema kuwa fedha hizo zitasaidia kufanikisha maandalizi ya michezo hiyo,huku akimuomba aendelee kuwa na moyo huo huo wa kujitoa kwa jamii.
TAZAMA PICHA👇👇
Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Hamisa Chacha akizungumza.
Kaimu Katibu wa Michezo ya Jadi Manispaa ya Shinyanga Leonard Mapolu akizungumza.
Mwenyekiti wa Michezo ya Jadi Manispaa ya Shinyanga Janeth Seseja akizungumza.
Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Hamisa Chacha (kushoto)akimkabidhi fedha Shilingi milioni 3, Mwenyekiti wa Michezo ya Jadi Manispaa ya Shinyanga Janeth Seseja,kwa niaba ya Mbunge Katambi.
Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Hamisa Chacha (kushoto)akimkabidhi fedha Shilingi milioni 3, Mwenyekiti wa Michezo ya Jadi Manispaa ya Shinyanga Janeth Seseja,kwa niaba ya Mbunge Katambi.
Picha ya pamoja ikipigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464