RC MACHA AKABIDHI MAGARI MAWILI SHUWASA,ATAKA YATUMIKE KUBORESHA HUDUMA ZA MAJI
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,amekabidhi magari mawili kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira kwa wananchi.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika leo Aprili 14,2025 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Amesisitiza kuwa magari hayo yatumike kwa malengo yaliyokusudiwa, na kusaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maji.
“Leo nazindua na kukabidhi rasmi magari haya mawili kwa SHUWASA. Nasisitiza yakatumike ipasavyo na yafanyiwe matengenezo ya mara kwa mara. Madereva pia wahakikishe wanaendesha kwa kufuata sheria za usalama barabarani,” amesema Macha.
Aidha, ametoa wito kwa watumishi wa SHUWASA kufanya kazi kwa bidii na kwa uzalendo mkubwa, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Amesisitiza pia watu ambao wamekuwa wakiiba maji wasihurumiwe bali wachukuliwe katua kali za kisheria.
Macha ametaja hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi, ambapo vijijini imefikia asilimia 68 na mijini asilimia 92. Na kwamba miradi inayoendelea ikikamilika, upatikanaji wa maji vijijini utaongezeka hadi asilimia 85 na mjini kufikia asilimia 100.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, amesema magari hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji, unaofadhiliwa kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa gharama ya Euro milioni 76, ambapo Euro milioni 1 imetolewa na Serikali ya Tanzania.
“Magari haya mawili thamani ya shilingi milioni 276.9, na yamenunuliwa kwa ajili ya kusaidia usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za mradi huu mkubwa wa kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira,”amesema Mhandisi Katopola.
Ameongeza kuwa uwepo wa magari hayo utasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mradi, kurahisisha ufuatiliaji wa karibu na kuchangia kufanikisha malengo ya mradi kwa wakati.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akikata Utepe kuzindua na kukabidhi Magari mawili kwa SHUWASA.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha (watatu kulia)akipongezana na Mkurugenzi wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola katika hafla ya kuwakabidhi Magari.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha (kulia)akimkabidhi ufunguo wa Gari Mkurugenzi wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akiwa kwenye Gari akijaribu kuendesha ambalo amelikabidhi SHUWASA.
Muonekano wa Magari Mawili ambayo yamekabidhiwa SHUWASA.
Watumishi wa SHUWASA.
Picha ya pamoja.
Picha ya pamoja.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464