TUMEKUJA KUJIRIDHISHA KAMA TARATIBU ZA MCHAKATO WA UGAWAJI WA JIMBO LA SOLWA ZILIZINGATIWA – MWITA
Mkurugenzi wa Daftari na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ndugu Stanslaus Mwita, amesema kuwa wamefika kujiridhisha na kuhakikisha kama taratibu na mchakato mzima wa mgawanyo wa Jimbo la Solwa ulifuatwa kulingana na maelekezo waliyotoa awali kabla ya kuanzishwa kwa zoezi hilo.
Stanslaus amesema hayo jana Aprili 23, 2025, wakati akiwasilisha taarifa ya INEC kwa wadau wa uchaguzi katika ukumbi wa mikutano uliopo kwenye jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Makamu Mwenyekiti wa INEC, Mheshimiwa Jaji wa Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha, na Katibu Tawala wa Mkoa huo, CP Salum Hamduni.
Wengine waliohudhuria ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mheshimiwa Peter Masindi (aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mheshimiwa Julius Mtatiro - Wakili), Mraribu wa Uandikishaji Mkoa wa Shinyanga Ndg. Bakari Kasinyo, Waheshimiwa Madiwani, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama vya Siasa pamoja na wataalamu mbalimbali wakiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Dkt. Kalekwa Kasanga.
"Tumekuja kujiridhisha na kuona kama taratibu na mchakato mzima wa mgawanyo wa Jimbo la Solwa ulifuatwa kulingana na maelekezo tuliyotoa kama INEC hapo awali kabla ya kuanzishwa kwa jambo hili. Hii ni sehemu tu ya mchakato, na si kwamba Tume imeridhia rasmi moja kwa moja," amesema Mwita.
Awali, akitoa salamu za INEC, Makamu Mwenyekiti Mhe. Jaji wa Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk alisema kuwa, pamoja na mambo mengine, uchambuzi wa kina ulifanyika kuhusu ombi hilo kwa kuzingatia vigezo muhimu ikiwemo kufanyika kwa vikao halali vya kisheria, idadi ya watu, mipaka ya kijiografia ya Jimbo la Uchaguzi, jina la Jimbo pamoja na mgawanyo wa Kata.
Kwa upande wao, wadau wa uchaguzi wa Shinyanga DC, akiwemo Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa Jimbo la Solwa, Ndg. Mashindike Bulanya, waliishukuru INEC kwa kuja kujiridhisha na kwamba, utekelezaji wa ugawaji wa Jimbo la Solwa unalenga kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kusogeza karibu, kwani kwa sasa jimbo hilo ni kubwa sana kijiografia, jambo linalopelekea baadhi ya maeneo kutopata huduma stahiki kwa wakati.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464