WAKULIMA,LIONGEZEENI THAMANI ZAO LA CHOROKO – RC MACHA

WAKULIMA,LIONGEZEENI THAMANI ZAO LA CHOROKO – RC MACHA

Shinyanga_rs

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewataka Wakulima wa Kijiji cha Mwamakaranga, Kata ya Iselamagazi Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kukipa kipaumbele kilimo cha zao la choroko na kulifanya kuwa zao la kibiashara ili kuongeza thamani yake na kuwawezesha kunufaika zaidi na zao hili ambalo linazidi kukua kwa kasi.

RC Macha ameyasema haya leo April 3, 2025 wakati wa mkutano wa hadhara na wakulima wa Mwamakaranga ambapo ulilenga kuonana, kujadili na kupata ufumbuzi wa changamoto wanazopitia wakulima hao sanjari na RC Macha kutembelea Ghala la kuhifadhi nafaka la Katemi lililopo kijijini hapo na kuona ufanisi wa kazi zake.

“Niwaombeni ndugu zangu Wakulima, pamoja na kulima mazao mengine lakini nawasisitiza sana mkipe kipaumbele kilimo cha zao la choroko na kulifanya zao hili kuwa la kibiashara zaidi ili kuliongezea thamani yake kwa kufanya hivyo kutawawezesha ninyi kunufaika zaidi kwani zao hili linazidi kukua kwa kasi sana hivi sasa” amesema RC Macha.

RC Macha pia ametumia nafasi hiyo kuwasisitiza kujisajili na kutumia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ambao unalenga kumnufaisha zaidi mkulima kwani mpaka sasa umeonesha waziwazi bei halisi ya zao husika na hivyo kumuepusha mkulima na walanguzi ambao wamekuwa wakiwakandamiza kutokana na bei zisizo halali.

Aidha ameongeza kuwa Serikali inakuja na utaratibu wa kuhakikisha zao la choroko linauzwa na kununuliwa kwenye maghala yaliyosajiliwa na yanayosimamiwa vizuri kwani hamu ya Serikali ni kuona wakulima ndio wanakuwa wanufaika wakubwa zaidi wa zao hili na mazao mengine ya kibiashara kuliko wafanyabiashara ambao kwa sasa ndio wanaonufaika zaidi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro (Wakili) amepokea maagizo ya RC Macha na kuahidi kuwa atashirikiana bega kwa bega na wakulima hao kuhakikisha zao la choroko linasonga mbele na kuleta maendeleo chanya kwa wakulima.

Awali baadhi ya wakulima walieleza changamoto wanazopitia kwenye zao hilo pamoja na changamoto zingine huku Serikali kupitia RC Macha amezipokea na kuahidi kwenda kufuatilia kwa undani zaidi na kuzitafutia suluhu.

Akihitimisha ziara yake RC Macha amewaomba na kuwasisitiza wakulima kuendelea kushirikiana kwa pamoja na Vyama vya Ushirika vya Kilimo na Masoko (AMCOS) ili kuliinua zao hili na kulifanya lizidi kupaa kimataifa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464