MWENYEKITI WA CCM MKOA WA SHINYANGA MABALA MLOLWA ATEMBELEA NA KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO SHULE YA SEKONDARI BUNAMBIYU KISHAPU


MWENYEKITI WA CCM MKOA WA SHINYANGA ATEMBELEA NA KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO SHULE YA SEKONDARI BUNAMBIYU KISHAPU


Na Mapuli Kitina Misalaba

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mabala Mlolwa, ametembelea na kukagua miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika shule ya sekondari Bunambiyu, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa wiki ya wazazi ngazi ya mkoa.

Uzinduzi huo unaofanyika leo Aprili 9, 2025 katika viwanja vya shule hiyo umehudhuriwa na mamia ya wanachama na wananchi, ukiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Shinyanga, John Siagi.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi wa miradi hiyo, Mhe. Mlolwa ameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha nyingi za maendeleo kwenye sekta ya elimu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Shule ya Sekondari Bunambiyu, Mzee Matata Joel, shule hiyo imepokea zaidi ya shilingi milioni 166.4 kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Katika mwaka wa fedha 2021/2022 tumepata fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa na ofisi; mwaka 2022/2023 tukajenga vyumba viwili vya madarasa; na mwaka 2023/2024 tumekamilisha vyumba viwili vya madarasa pamoja na matundu manne ya vyoo,” amesema Mzee Matata.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kati ya shilingi 166,400,000 zilizotolewa na serikali, kiasi cha shilingi 165,892,880.50 kimetumika katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa mafanikio makubwa.

Mara baada ya ukaguzi huo, viongozi wa chama wakiwemo Mhe. Mlolwa na viongozi wengine wa Jumuiya ya Wazazi wamepanda miti katika mazingira ya shule hiyo kama ishara ya utunzaji wa mazingira na kuongeza mvuto wa shule.

Viongozi wengine walioungana na Mwenyekiti Mlolwa katika uzinduzi huo ni pamoja na Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Odilia Batimayo; Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo Richard Masele; Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Anord Makombe pamoja na viongozi wengine wa chama na jumuiya hiyo.

Maadhimisho ya wiki ya wazazi ngazi ya mkoa yanaendelea kwa kutoa elimu kwa wazazi juu ya masuala ya malezi, maadili, elimu, afya na maendeleo ya jamii kwa ujumla.







Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464