DCEA YAKAMATA KILO 4,568 ZA DAWA ZA KULEVYA, YAZUIA TANI 14 ZA KEMIKALI BASHIRIFU KUINGIA NCHINI

Dar es Salaam, April 24, 2025.
Mwezi Machi na Aprili, 2025 Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola imefanya operesheni Katika mikoa ya Dar es Salaam, shinyanga, Tabora, Tanga, Songwe, Mbeya na Arusha na kufanikiwa kuzuia tani 14 za kemikali bashirifu zilizokuwa ziingizwe nchini kinyume cha sheria, kukamata pakti 10 za pipi zenye uzito wa gramu 174.77 zilizotengenezwa kwa kutumia bangi, kukamata kilogramu 4,568 za dawa mbalimbali za kulevya, kuteketeza ekari 178 za mashamba ya bangi pamoja na kushikilia magari saba, pikipiki tano na bajaji moja vilivyohusika kwenye uhalifu huo. Jumla ya watuhumiwa 35 wamekatwa na taratibu za kisheria zinaendelea dhidi yao.

Kwa kushirikiana na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Duniani (INCB) na mamlaka nyingine za udhibiti, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilibaini na kuzuia kilogramu 4,000 za kemikali aina ya 1-Boc-4-piperidone na kilogramu 10,000 za kemikali aina ya Acetic anhydride zilizokuwa ziingizwe nchini kutokea bara la Asia bila kuwa na vielelezo vinavyoonesha matumizi ya kemikali hizo. Endapo kemikali hizi zingeingizwa nchini na kuchepushwa zingeweza kutumika kutengeneza dawa za kulevya aina ya fentanyl na heroin.

Mathalani, kilogramu 4,000 za kemikali aina ya 1-Boc-4-piperidone zinaweza kutengeneza kilogramu 8,000 za dawa za kulevya aina ya fentanyl. Matumizi ya kiasi hicho cha dawa za fentanyl ambazo zingezalishwa zingeweza kusababisha vifo kwa watumiaji bilioni nne (4) ikizingatiwa kwamba, kilogramu moja (1) ya dawa hizo inaweza kusababisha vifo kwa watu 500,000 kutegemea na uzito, afya, na historia ya mtumiaji (miligramu mbili (2) inaweza kusababisha kifo kwa mtu mmoja).

Kemikali aina ya acetic anhydride inaweza kutumika katika mchakato wa kutengeneza dawa za kulevya aina ya heroin. Hivyo, kiasi cha kilogramu 10,000 kilichozuiliwa kingeweza kutumika kutengeneza kilogramu 3,704 za heroin. Aidha, kemikali hiyo inaweza kutumika kuzalisha kemikali nyingine bashirifu ambazo zinaweza kutumika kuzalisha dawa za kulevya za mandrax na methamphetamine. Uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa unaendelea ili kubaini mitandao zaidi ya usafirishaji haramu wa kemikali bashirifu zinazoweza kuchepushwa na kutengeneza dawa za kulevya.

Katika operesheni zilizofanyika mkoani Mbeya, raia wa Uganda Herbert Kawalya mwenye hati ya kusafiria Na. B00132399 na mmiliki wa kampuni ya Hoxx Wells Lux Tour Limo, alikamatwa akiwa na pakti 10 za pipi zenye uzito wa gramu 174.77 zilizotengenezwa kwa dawa za kulevya aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu ya tetrahydrocannabinol (THC). Ukamataji huo, ulikwenda sambamba na ukamataji wa gari ndogo aina ya Mercedes Benz yenye namba za usajili MG 33 BM GP iliyokuwa inasafirisha pipi hizo kuingia nchini kutokea Afrika Kusini. Utengeneza wa pipi hizi zenye kiwango kikubwa cha sumu aina ya THC ni ushahidi wa nia ovu ya wahalifu kulenga kuharibu vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.

Aidha, katika tukio lingine mkoani Mbeya, zilikamatwa kilogramu 1,658 za bangi aina ya skanka na kilogramu 128.7 za bangi zilizokuwa zinaingizwa nchini kutoka nchini Malawi.

Operesheni zilizofanyika Jiji Dar es Salaam, zilifanikisha ukamataji wa kilogramu 220.67 za bangi aina ya skanka katika kata ya Chanika zikiwa zimefichwa chooni huku kilogramu 11 zikikamatwa eneo la ukaguzi wa mizigo kwenye bandari ya kuelekea Zanzibar.

Katika operesheni zilizofanyika mikoa ya Arusha, Tanga, na Manyara zilikamatwa kilogramu 733.74 za dawa ya kulevya aina ya methamphetamine, kilogramu 91.62 za heroin, kilogramu 692.84 za mirungi iliyokuwa inaingizwa kutokea nchini Kenya na kilogramu 115.05 za bangi pamoja na kuteketeza ekari mbili (2) za mashamba ya bangi. Vilevile, operesheni zilizofanyika katika Wilaya ya Uyui na Nzega mkoani Tabora, kilogramu 845 za bangi zilikamatwa na ekari 176 za mashamba ya bangi ziliteketezwa. Kadhalika, kilogramu 98.35 za dawa za kulevya aina ya bangi zilikamatwa katika operesheni zilizofanyika wilayani Kahama na Shinyanga.

Udhibiti wa dawa za kulevya na kemikali bashirifu uliofanyika, umezuia athari kubwa ambazo zingejitokeza kiafya, kijamii, kiuchumi na kimazingira ikiwemo kuongezeka kwa dawa za kulevya mtaani. Pia, ukamataji huu umesaidia kuokoa nguvu kazi ya Taifa ambayo ingeangamia endapo dawa hizo zingeingizwa mitaani.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) inatoa wito kwa wananchi kuendeleza ushirikiano kwa kutoa taarifa mapema wanapohisi au kuona uwepo wa shughuli zinazohusiana na biashara au uzalishaji wa dawa za kulevya katika maeneo yao kupitia kituo chetu cha taarifa na huduma kwa kupiga namba 119 bure. Vilevile, wazazi na walezi mnahimizwa kuwa makini na kufuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wenu ikiwa ni pamoja na kuwaasa wajiepushe na mazingira na sababu zozote zinazoweza kuwaingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

Pia, tunazikukumbusha kampuni zinazojihusisha na biashara na matumizi ya kemikali za viwandani na kilimo kuzingatia matakwa ya sheria za nchi na kuepuka kushirikiana na magenge ya kihalifu kusafirisha kemikali bashirifu ambazo zinaweza kuchepushwa na kutengeneza dawa za kulevya.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA
📧 cg@dcea.go.tz

🌐 www.dcea.go.tz



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464