Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imepongeza hatua ya kuanzishwa kwa maabara ya kujifunzia somo la Jiografia katika Shule ya Sekondari Shinyanga, iliyopo Kata ya Mwadui Lohumbo.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mhe. Francis Manyanda, alitoa pongezi hizo tarehe 14 Aprili 2025 wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo, akisema kuwa maabara hiyo ni chachu ya kuongeza uelewa wa wanafunzi kupitia ujifunzaji wa vitendo.
"Niwapongeze sana walimu kwa ubunifu mkubwa wa kuwaongezea maarifa watoto wetu kupitia mafunzo ya vitendo. Napendekeza Afisa Elimu Msingi ahimize walimu wa shule zingine kuja kujifunza hapa ili waweze kuanzisha maabara kama hizi katika maeneo yao," alisema Mhe. Manyanda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Mazingira ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwamashele, Mhe. Lucas Daudi Nkende, alisema ni vyema wanafunzi kutoka shule nyingine wakaletwa kwa makundi kujifunza kwa vitendo kuhusu mada mbalimbali za somo la Jiografia, ili kuinua ufaulu katika wilaya nzima.
Afisa Elimu Sekondari, David Mashauri, alieleza kuwa Halmashauri inaendelea kuhamasisha uanzishwaji wa maabara kama hiyo katika shule zote, ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa wizara wa kuimarisha ujifunzaji wa somo hilo kwa vitendo.
"Niwaombe waheshimiwa madiwani, mnapotembelea maeneo yenu, waambieni wazazi juu ya umuhimu wa elimu na kuwa tayari kuchangia gharama ndogo za usafiri ili watoto wao waweze kufika hapa kujifunza," aliongeza Mashauri.
Mkuu wa Shule ya Shinyanga Sekondari, Mwl. Bernard Ishengoma, alisema kuwa shule hiyo ilikuwa ya kwanza kuanzisha maabara ya Jiografia Kishapu tangu mwaka 2024. Hata hivyo, alibainisha kuwa bado kuna uhitaji wa vifaa vya kisasa kama projekta na runinga ili kurahisisha ufundishaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
"Tunashukuru sana Halmashauri kwa ushirikiano mkubwa waliotupa. Tunaendelea kuboresha, lakini bado tunahitaji msaada zaidi ili kuboresha mazingira ya kujifunzia wanafunzi wetu," alisema Mwl. Ishengoma.
Katika kikao cha majumuisho kilichofanyika Aprili 15, 2025, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Willium Jijimya, aliiagiza Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kupitia Idara ya Elimu kuwapa kipaumbele wanafunzi wa madarasa ya mitihani—kidato cha pili na cha nne—kwenda kufanya ziara za mafunzo kabla ya wengine, sambamba na kuendelea kuboresha maabara hiyo.
Shule hiyo ya bweni ya wavulana iliyopo Kijiji cha Wizunza ina jumla ya wanafunzi 878, wakiwemo 118 wenye mahitaji maalum, na walimu 34.
Baadhi ya zana za kujifunzia kwa vitendo somo la jiografia vilivyopo shule ya wavulana Shinyanga sekondari iliyoko Kata ya Mwaduhi Luhumbo Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga
Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe.Francis Manyanda
Mwenyekiti wa kamati ya uchumi na mazingira ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwamashele Mhe.Lucas Daud Nkende akizungumza kwenye ziara ya kikazi ya kamati ya fedha,utawala na mipango katika shule ya sekondari Shinyanga iliyoko Wilayani humo Aprili 14,2025
Mkuu wa shule ya sekondari Shinyanga iliyoko Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Mwl. Bernard Ishengoma
Afisa elimu sekondari Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga David Mashauri akizungumza
Picha ya pamoja ya kamati ya fedha,utawala na mipango Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga na uongozi wa shule ya sekondari Shinyanga iliyoko Wilayani humo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464