MFANYABIASHARA AKAMATWA KWA KUKUTWA NA DIRA ZA MAJI ZILIZOIBWA KAHAMA


MFANYABIASHARA AKAMATWA KWA KUKUTWA NA DIRA ZA MAJI ZILIZOIBWA KAHAMA

Na Salvatory Ntandu,KAHAMA

Mfanyabiashara wa vyuma chakavu, Rajabu Msimbe, mkazi wa Mtaa wa Majengo wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa na dira mbili za maji mali ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA).

Dira hizo zilikuwa zimefungwa pamoja na mzigo wa vyuma chakavu katika moja ya maghala ya ofisi yake, huku zikiwa zimefichwa kwa ustadi mkubwa.

Tukio hilo jana baada ya Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Kahama KUWASA kufanya msako kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa za siri juu ya wizi wa Dira hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Uhusiano wa KUWASA, John Mkama, amesema kuwa baada ya taarifa hizo kupokelewa, walifanya msako uliofanikisha kukamatwa kwa Msimbe na kukutwa na dira hizo ndani ya ofisi yake.

“Rajabu alikana kuhusika moja kwa moja akidai kuwa hakuwapo ofisini wakati mzigo huo ulipokelewa, na kwamba walihusika ni vijana wake waliokuwa kazini. Hata hivyo, kutokana na ukubwa wa tatizo hili, lazima afikishwe kwenye vyombo vya sheria ili kusaidia uchunguzi,” amesema Mkama.

Kwa mujibu wa Mkama, wizi wa dira za maji umekithiri katika mitaa ya Nyahanga, Malunga na Majengo, hali inayosababisha hasara kubwa kwa mamlaka hiyo. Alisema kuwa katika kipindi cha Oktoba 2024 hadi Aprili 2025, jumla ya dira 210 zimeibwa na watu wasiojulikana.

“Thamani ya dira moja ni Shilingi 120,000. Kwa dira 210 ni zaidi ya Shilingi milioni 25 ambazo mamlaka imepoteza kutokana na wizi huu. Hii ni changamoto kubwa kwa huduma ya maji kwa wananchi,” ameongeza Mkama.

Katika maelezo yake ya awali, Msimbe alijitetea kwa kusema kuwa hana taarifa kuhusu upatikanaji wa dira hizo kwani vijana wake walinunua mzigo huo bila kujua kilichokuwemo. Alisema tayari walikuwa wamepewa elimu na Serikali kutonunua dira za maji kama vyuma chakavu, na aliomba kusamehewa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo, Emmanuel Nangale, alithibitisha kukamatwa kwa Msimbe na kuwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa kuhusu wahalifu wanaohujumu miundombinu ya maji.

“Matukio ya wizi wa dira za maji katika Mtaa wa Majengo yameongezeka. Mpaka sasa kuna zaidi ya matukio 10 yaliyoripotiwa, na wahusika wakuu ni wanunuzi wa vyuma chakavu. Wakitokomezwa, wizi huu utadhibitiwa,” amesema Nangale.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464