Taarifa rasmi iliyotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeeleza kuwa awali tukio hilo lilipangwa kufanyika tarehe 29 Aprili 2025 katika Ukumbi wa Mabele, Mabeyo Complex, jijini Dodoma, lakini limehamishwa kwa sababu za kiutendaji zisizoweza kuepukika.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye tuzo hizi zinabeba jina lake, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika hafla hiyo kubwa ya kitaifa. Tuzo hizi zinatambua mchango wake mkubwa katika kuhimiza maendeleo kupitia tasnia ya habari.
TAMWA na TCRA wameomba radhi kwa usumbufu wowote uliosababishwa na mabadiliko haya na kuwaomba wadau, washiriki na waalikwa kuendelea na maandalizi ya kushiriki hafla hiyo muhimu inayolenga kuthamini mchango wa wanahabari katika maendeleo ya taifa.
