Hafla ya utoaji wa Tuzo za Uandishi wa Habari kwa Maendeleo zinazojulikana kama Samia Kalamu Awards 2025 sasa itafanyika jijini Dar es Salaam tarehe 5 Mei 2025, tofauti na ratiba ya awali iliyopangwa tukio hilo kufanyika tarehe 29 Aprili 2025 katika Ukumbi wa Mabele, Mabeyo Complex, jijini Dodoma.
Taarifa rasmi iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeeleza kuwa mabadiliko haya yamesababishwa na sababu za kiutendaji zisizoweza kuepukika.
“Waalikwa wote watatumiwa mialiko mipya itakayotolewa yenye maelezo kamili kuhusu eneo na ratiba ya tukio,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Mgeni Rasmi anayetarajiwa kuhudhuria hafla hiyo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia tuzo hizo zinabeba jina lake kwa kutambua mchango wake katika kuhimiza maendeleo kupitia vyombo vya habari.
TAMWA na TCRA wamewaomba radhi washiriki wote kwa usumbufu wowote uliojitokeza kutokana na mabadiliko hayo, huku wakiwataka kuendelea na maandalizi ya kushiriki hafla hiyo muhimu ya kutambua mchango wa wanahabari katika maendeleo ya taifa.
