Na WMJJWM Dodoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameitaka jamii kuimarisha ushirikiano ili kuzuia Mtoto Kuishi na kufanya kazi mtaani katika maeneo ya miji.
Waziri Dkt. Gwajima amesema katika kipindi cha Julai 2024 hadi Machi 2025 jumla ya Watoto 8,372 (Me 4,218 Ke 4,154) wanaoishi na kufanya kazi mtaani waliokolewa na kupatiwa huduma mbalimbali ambazo watoto 1056 wako katika Makao ya Watoto na Nyumba Salama, 86 wako kwa Walezi wa kuaminika na waliobakia waliunganishwa na familia zao.
Waziri Dkt. Gwajima ameeleza kwamba sababu kubwa zinazopelekea watoto kukimbilia mtaani ni pamoja na na umasikini wa kaya, migogoro ya familia, migogoro ya ndoa, ukatili dhidi ya watoto, vifo vya wazazi/wategemezi, utoro na kushindwa masomo shuleni, athari za kukua kwa miji na athari za makundi rika.
"Afua zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na changamoto ya watoto kuishi na kufanya kazi mtaani ni pamoja na utatuzi wa migogoro ya ndoa kupitia Ofisi za Ustawi wa Jamii nchi nzima, Uratibu wa huduma kwa manusura wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto na Huduma ya matunzo na malezi kwa Watoto inayotolewa kwenye Makao mawili ya Watoto yanayomilikiwa na kuendeshwa na Serikali", amesema Dkt Gwajima.
Aidha Dkt. Gwajima ameeleza kwamba kwa sasa Serikali itajikita zaidi kwenye mikakati ya kuziba mianya inayosababisha watoto kwenda kuishi mtaani kupitia modeli ya kitaalam ya "Close the Tap" kwa kushughulikia changamoto za kifamilia na kiuchumi zinazowasukuma watoto kuingia mtaani.
“Serikali imeandaa matukio ya kuelimisha jamii juu ya tatizo la Watoto Wanaoishi na Kufanya Kazi Mtaani kwa kufanya Kampeni ya Kumuokoa Mtoto Kutoka kuishi Mtaani iliyoanza tarehe 07 Aprili 2025, Kufanya mijadala na midahalo ya kijamii kwa njia mbalimbali ili kuwafikia wananchi na tarehe 11 Aprili, 2025, katika mkoa wa Mtwara, Kata ya Chikongola, kutakuwa na mdahalo wa ana kwa ana na wananchi kuhusu wajibu wa familia na jamii katika kuzuia watoto kwenda mitaani” amesema Dkt Gwajima.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkuu wa Dodoma ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Janeth Mayanja amesema maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto Anayeishi na Kufanya Kazi Mtaani ni moja ya utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto Duniani kupitia Hati ya Maoni ya Jumla Na. 21 ya mwaka 2017 kuhusu hali ya watoto waliopo mtaani.
“Tunajua Wizara ina jukumu la kuratibu na kusimamia utolewaji wa huduma kwa Watoto Walio katika Mazingira Hatarishi wakiwemo Watoto Wanaoishi na Kufanya Kazi Mtaani kama Mkoa tunashirikiana kuwa kuhakikisha jukumu hili linatekelezwa kwa kuweka mazingira wezeshi kupitia Sera, Sheria, Kanuni, Miongozo na Mikakati mbalimbali ya kulinda haki za watoto, kuimarisha mifumo ya uangalizi na usimamizi wa ustawi na ulinzi wa watoto.”amesema Mhe. Janeth.
Kilele cha Maadhimisho haya yatafanyika katika ukumbi wa VETA mkoani Mtwara, yakihusisha viongozi wa Serikali, wadau wa maendeleo na wananchi Aprili 12, 2025.